
Yanga SC vs Kengold SC: Vita ya Mabingwa Dhidi ya Walio na Njaa ya Ushindi
Katika dimba la KMC Complex leo jioni, macho na masikio ya mashabiki wa soka yatakuwa yamelenga pambano kali kati ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans SC (Yanga), dhidi ya Kengold SC katika mchezo wa raundi ya 17 ya NBC Premier League. Wakati Yanga ikisaka kuendeleza ubabe wake kileleni mwa ligi, Kengold inapambana kwa udi na uvumba kujinasua kutoka kwenye janga la kushuka daraja.
Yanga SC: Ubabe Unaoendelea
Baada ya kuichakaza Kagera Sugar kwa mabao 4-0 wiki iliyopita, Yang a inaingia uwanjani ikiwa na morali ya juu na rekodi ya ushindi wa mechi sita mfululizo. Chini ya kocha Sead Ramovic, kikosi hiki kimekuwa moto wa kuotea mbali, kikiongozwa na nyota wake kama Clement Mzize, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, na Kennedy Musonda Romelu. Kwa mashabiki wa Wananchi, matarajio ni kuona timu yao ikiendeleza rekodi ya ushindi na kuzidi kutanua pengo la alama kileleni.
Kengold SC: Mapambano ya Kupona
Kwa upande mwingine, Kengold SC inaingia uwanjani ikiwa katika hali ngumu, baada ya kupoteza michezo minne mfululizo. Ikiwa na pointi sita pekee baada ya mechi 16, hatima yao inazidi kuwa mashakani ikiwa hawatabadili mwenendo wao. Katika jitihada za kuimarisha kikosi, uongozi wa Kengold ulifanya usajili mkubwa dirisha dogo kwa kuongeza wachezaji wazoefu kama Bernard Morrison, Obrey Chirwa, na Kelvin Yondani. Aidha, kocha mpya Vladislav Heric amepewa jukumu zito la kuinusuru timu kutoka katika janga la kushuka daraja.
Kikosi cha Yanga vs Kengold Leo
Kikosi rasmi cha Yanga kitakachoshuka dimbani kitatajwa saa 9:00 alasiri, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona mastaa watakaopewa majukumu ya kuhakikisha ushindi unapatikana. Kwa upande wa Kengold, wanatarajiwa kuingia uwanjani na mbinu mpya za kuhakikisha wanazuia Yanga kupata mabao kirahisi na, ikiwezekana, kusaka matokeo chanya.

Be the first to comment