
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Jacob John Mkunda, ametangaza fursa za kujiunga na Jeshi hilo kwa vijana waliomaliza elimu ya sekondari hadi vyuo vikuu.
Taarifa hiyo imetolewa leo, Aprili 30, 2025, katika Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo Msalato, jijini Dodoma, kupitia Msemaji wa JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda, kwa niaba ya Jenerali Mkunda. Kanali Ilonda ameeleza kuwa nafasi hizo zinahusu vijana wenye elimu ya:
- Kidato cha Nne au Sita: Umri usiozidi miaka 24
- Stashahada: Umri usiozidi miaka 26
- Elimu ya Juu (Shahada): Umri usiozidi miaka 27
- Madaktari Bingwa wa Binadamu: Umri usiozidi miaka 35
Kanali Ilonda amebainisha kuwa maombi yote yanapaswa kuandikwa kwa mkono, na muda wa kuwasilisha maombi hayo ni kuanzia kesho Mei 1, 2025 hadi Mei 14, 2025. Maombi yawasilishwe yakiwa yameambatishwa na:
- Nakala ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) pamoja na namba yake
- Nakala ya cheti cha kuzaliwa
- Vyeti vya shule au chuo husika
- Namba ya simu inayopatikana kwa urahisi kwa ajili ya mawasiliano
Nafasi za kazi Jeshi la Wananachi Tanzania JWTZ
Aidha, Kanali Ilonda ametoa onyo kwa wananchi kuepuka kudanganywa na matapeli wanaoweza kutumia fursa hiyo kwa nia ya kujipatia fedha kwa ahadi ya kuwapata nafasi jeshini.
“Ninatoa angalizo kwa wananchi: hakuna nafasi ya kujiunga na Jeshi kwa kutoa fedha. Msikubali kutapeliwa,” amesisitiza Kanali Gaudentius Ilonda.
Be the first to comment