Wasifu wa Papa Francis: Maisha, Safari yake ya Kiroho, na Habari za Kifo chake 1936 – 2025

Wasifu wa Papa Francis

Papa Franci’s, ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Buenos Aires, Argentina. Yeye ndiye Papa wa kwanza kutoka Amerika Kusini, na pia ni mwanachama wa kwanza wa Shirika la Yesu (Jesuits) kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki.

Maisha ya Awali ya Papa Francis

Baba yake, Mario Bergoglio, alikuwa mhasibu kwenye shirika la reli, na mama yake, Regina Sivori, alikuwa mama wa nyumbani. Katika ujana wake, Papa Francis alifanya kazi nyingi – ikiwa ni pamoja na kuwa mlinzi wa baa ili kujilipia gharama za shule.
Alisomea kemia, lakini baadaye akaamua kujiunga na maisha ya kidini. Mwaka 1958, alijiunga rasmi na Shirika la Yesu. Aliweka nadhiri za muda mwaka 1960, na akapadrishwa tarehe 13 Desemba 1969.

Kazi za Kidini na Uongozi

Baada ya kupata upadrisho, alihudumu katika parokia mbalimbali. Mwaka 1992, aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Buenos Aires, na baadaye mwaka 1998, akawa Askofu Mkuu wa mji huo.
Papa Francis alijipatia sifa kwa kupigania haki za maskini na wanyonge. Alihudumu pia kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Argentina kuanzia mwaka 2005 hadi 2011.

Uchaguzi Wake Kama Papa

Tarehe 13 Machi 2013, baada ya kujiuzulu kwa Papa Benedikto XVI, Jorge Bergoglio alichaguliwa kuwa Papa mpya wa Kanisa Katoliki. Alipochaguliwa, alichagua jina Francis, kumuenzi Mtakatifu Francis wa Assisi – aliyefahamika kwa maisha ya unyenyekevu na huduma kwa maskini.
Waraka wake wa kwanza kama papa uliitwa “Lumen Fidei”, uliolenga kueleza maana ya imani kwa Wakatoliki.

Sifa na Mtazamo wa Papa Francis

Papa Francis anaheshimika kwa unyenyekevu wake. Tofauti na viongozi wengi, aliendelea kuishi maisha rahisi, akiepuka anasa. Amekuwa kiongozi anayejali mazingira, maskini, na wale waliopuuzwa katika jamii.
Barua yake maarufu ya mwaka 2015, “Laudato si’”, ilisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Habari za Kifo cha Papa Francis – April 21, 2025 ~ Wasifu wa Papa Francis

Kwa masikitiko makubwa, Kanisa Katoliki na ulimwengu mzima umeupoteza kiongozi shupavu na mwenye upendo mkubwa kwa watu.
Papa Franc’is amefariki dunia leo, Aprili 21, akiwa nyumbani kwake mjini Vatican. Alikuwa na miaka 88. Kifo chake kimetokea akiwa katika mapumziko ya kawaida.
Tunaungana na mamilioni ya waumini duniani kumwombea apumzike kwa amani.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*